IQNA

Kuongezeka kwa Chuki dhidi ya Uislamu nchini Brazil

14:28 - February 16, 2026
Habari ID: 3481942
IQNA – Kumeshuhudiwa visa kadhaa vya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Waislamu nchini Brazil, hali inayoashiria kuongezeka kwa tatizo la Chuki Dhidi ya Uislamu katika taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Wasl, shambulio la kibaguzi na lenye misingi ya chuki ya kidini lilitokea wiki iliyopita katika mji wa Foz do Iguaçu, ambapo wanawake wawili Waislamu walishambuliwa kimwili na kutukanwa kwa maneno ndani ya kituo cha ununuzi.

Tukio hilo, lililotokea Alhamisi, Februari 12, si tukio la pekee, bali linaakisi kuongezeka kwa hali ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Brazil, pamoja na athari za migogoro ya kimataifa na kauli za chuki dhidi ya wageni kwa jamii za Waislamu.

Wanawake hao wawili, mmoja  mwenye asili ya Syria na mwingine mwenye asili ya Lebanon, ni wanachama wa jamii ya Waarabu Waislamu katika mji wa Foz do Iguaçu. Walishambuliwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 33 ndani ya kituo cha ununuzi cha Cataratas GL.

Mshambuliaji huyo alijaribu kuvua hijabu ya mmoja wa wanawake hao, akawashambulia, na kutoa matusi ya kibaguzi na kidini dhidi yao kwa sababu ya mavazi yao na imani yao ya Kiislamu.

Baadhi ya wanunuzi waliingilia kati kwa hekima ili kutuliza hali hiyo na kumzuia mshambuliaji hadi polisi walipofika. Baadaye, mwanaume huyo alikamatwa kwa tuhuma za shambulio na ubaguzi wa rangi. Polisi walieleza kuwa alikuwa na historia ya vitendo vya kibaguzi na vinavyochochewa na chuki ya kidini, ikiwa ni pamoja na kuvuruga sherehe za kidini.

Uongozi wa kituo cha ununuzi cha Cataratas JL ulitoa taarifa rasmi kulaani vikali tukio hilo na kusisitiza dhamira yao ya kufuata taratibu za kushughulikia matukio kama hayo, ikiwemo kumzuia mhusika na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola. Pia walisisitiza upinzani wao thabiti dhidi ya aina yoyote ya vurugu za kimwili au maneno dhidi ya wanawake, na dhidi ya vitendo vyovyote vya chuki ya kidini, kikabila au kijinsia.

Habari inayohusiana:

Tukio hili linafunua sura mbaya ya kuongezeka kwa Chuki Dhidi ya Uislamu nchini Brazil. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni kuhusu chuki dhidi ya Uislamu nchini humo, takribani asilimia 60 ya Waislamu wa Brazil wamekumbana na aina fulani ya kutovumiliwa kidini. Wanawake Waislamu wanaovaa hijabu wako katika hatari zaidi ya kulengwa.

Brazil ni nchi isiyo na dini rasmi (secular state), kwa mujibu wa katiba yake ya mwaka 1988, ambayo inahakikisha usawa wa kidini. Aidha, Sheria Na. 9.459 ya mwaka 1997 inaharamisha vitendo au uchochezi wa ubaguzi unaotokana na rangi, rangi ya ngozi, asili ya kikabila, dini au utaifa, na inaweka adhabu ya kifungo cha kati ya mwaka mmoja hadi mitatu gerezani.

3496432

captcha