
Hujjat-ul-Islam Hamid Reza Arbab Soleimani, ambaye pia ni mkuu wa Kituo Kikuu cha Qur'ani na Etrat katika Wizara ya Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu ya Iran, aliorodhesha malengo ya kimkakati ya maonyesho hayo kama ifuatavyo:
kutoa umuhimu maalumu kwa taasisi ya familia kwa lengo la kuendeleza mtindo wa maisha wa Kiirani-Kiislamu; kuzingatia kwa upekee suala la familia sambamba na Qur'ani Tukufu; na kutenga sehemu maalumu kwa Nahj al-Balagha, Sahifa Sajjadiyya, Mahdawiyya, na Ghadir.
Pia alisisitiza umuhimu wa diplomasia ya Qur'ani kwa kuwaalika wanazuoni, wasanii na wanaharakati kutoka ulimwengu wa Kiislamu, pamoja na kutumia teknolojia mpya na uwezo wa kielimu unaotokana na maarifa.
Alitoa kauli hizo katika hafla iliyofanyika mjini Tehran siku ya Jumatatu kwa ajili ya kufunua bango rasmi la maonyesho ya mwaka huu.
Kaulimbiu ya toleo hili ni “Iran chini ya ulinzi wa Qur'ani”, ambayo, kwa mujibu wake, si jina tu bali ni mwelekeo wa kiustaarabu na nguzo ya utambulisho wa taifa. “Qur'ani ni mhimili wa mshikamano wetu wa kitaifa na mamlaka yetu ya kitamaduni, na hatupaswi kamwe kusahau ukweli huu,” alisema.
Hujjat-ul-Islam Arbab Soleimani alibainisha kuwa Maonyesho ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran yatafanyika kwa muda wa wiki mbili kuanzia Februari 20, katika ukumbi mkuu wa Msalla wa Imam Khomeini (RA).
Alisema maonyesho hayo yatapokea wageni kila siku kuanzia saa 10:00 jioni hadi saa 5:00 usiku.
Aliongeza kuwa mada kuu za maonyesho hayo ni pamoja na:
Qur'ani na kujenga matumaini pamoja na uhai wa kijamii, Qur'ani, mshikamano wa kitaifa na umoja wa Kiislamu, Qur'ani na Mapinduzi ya Kiislamu, Qur'ani, swala na msikiti kama kipimo cha maadili, Qur'ani na kurekebisha mtindo wa matumizi, Qur'ani, staha na hijabu, Qur'ani na Mtume Mtukufu (SAW) kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 1500 ya kuzaliwa kwa Mtume wa Uislamu, Qur'ani na kuamrisha mema na kukataza maovu, Qur'ani na Nahj al-Balagha, Qur'ani na Sahifa Sajjadiyya, Qur'ani na Mahdawiyya, Qur'ani na Ghadir, Qur'ani na maisha ya Manabii na Maimamu Waliotakaswa (AS), na Qur'ani na sayansi za kisasa.

Kwa mujibu wa afisa huyo, jumla ya eneo la maonyesho ni takribani meta za mraba 16,000.
Alisema maonyesho hayo yameandaliwa kupitia makao makuu na kamati za utekelezaji 12, sehemu 11 za maonyesho zenye mwelekeo wa kitamaduni na kielimu, pamoja na sehemu tatu za maduka zenye mwelekeo wa uchumi wa kitamaduni. Maonyesho hayo pia yatakuwa na zaidi ya vikundi vidogo 70, matukio, na vibanda maalumu.
Alisisitiza kuwa: “Maonyesho ya Qur'ani ni fursa muhimu ya kuitambulisha Qur'ani Tukufu na wanaharakati wa Qur'ani kwa kina zaidi, kubadilishana uzoefu, na kuwasilisha mafanikio mapya katika nyanja ya Qur'ani na Etrat.”
Aliongeza kuwa tukio hilo linaweza kuwa jukwaa la kitaifa na kimataifa la kutambulisha kazi na mafanikio hayo.
Pia akizungumza katika hafla hiyo, Asghar Amirnia, makamu wa rais mtendaji wa Maonyesho ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani, alisema kuwa wanafikra, wanazuoni na wasanii kutoka Indonesia, Misri, Oman, Kuwait, Uturuki, Pakistan, Bahrain, China, Afghanistan, Algeria, Romania, Iraq, Bosnia na Herzegovina, Kazakhstan na Tunisia wametangaza utayari wao wa kushiriki katika maonyesho hayo.
Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran hufanyika kila mwaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, yakiratibiwa na Wizara ya Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu ya Iran.
Habari inayohusiana:
Kupitia programu mbalimbali kama vikao maalumu, warsha za elimu, mikusanyiko ya Qura'ni, pamoja na shughuli mahsusi kwa watoto na vijana, tukio hili la kimataifa linalenga kuendeleza mafundisho na shughuli za Qur'ani.
Maonyesho hayo pia yanatumika kama jukwaa la kuonesha mafanikio mapya ya Qur'ani nchini Iran, pamoja na bidhaa mbalimbali zinazolenga kueneza na kuhudumia Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani.
4334725