IQNA

Urithi Ulio Hatarini: Juhudi za Gaza Kuokoa Hazina za Kale za Msikiti Mkuu wa Omari

14:15 - February 25, 2026
Habari ID: 3481992
IQNA – Kwa karne nyingi, Msikiti Mkuu wa Omari umesimama kama mlinzi kimya wa historia ya kielimu ya Gaza, hukoo Palestina huku maktaba yake ikihifadhi maandiko ya kale yaliyoandika simulizi za kupanda na kushuka kwa ustaarabu mbalimbali.

Leo hii, ndani ya mabaki yenye vumbi ya moja ya maktaba kongwe zaidi katika Ukanda wa Gaza, kundi la  Wapalestina waliojitolea linafanya kazi kwa bidii kuokoa kilichosalia cha urithi wao wa kitamaduni na kidini.

Maktaba ya Msikiti Mkuu wa Omari imeharibiwa vibaya kufuatia vita vikali vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza, vilivyoanza Oktoba 2023, na kuacha uharibifu mkubwa uliogusa maeneo ya makazi, pamoja na vituo vya dini na utamaduni.

Msikiti huo, uliopo katika Mji wa Kale wa Gaza, sasa unasimama katika hali ya karibu kuangamia kabisa, huku maktaba yake ikiwa imejaa vifusi, mavumbi na mabaki ya uharibifu.

 “Nilishtuka sana nilipoona kiwango cha uharibifu ndani ya maktaba,” alisema Haneen AlAmsi katika mahojiano na TRT, akiongeza kuwa mandhari hiyo ya maangamizi ilimsukuma kujiunga na juhudi za kuanzisha mpango wa kurejesha urithi huo.

AlAmsi, ambaye ni mkuu wa Taasis ya Kujitolea ya Eyes on Heritage, alisema kuwa sehemu ya magharibi ya maktaba iliteketezwa kwa moto baada ya msikiti kulengwa na majeshi ya Israel, hali iliyosababisha uharibifu usioweza kurekebishwa.

 “Maktaba ilikadiriwa kuwa na takriban vitabu 20,000, lakini sasa tumebakiwa na chini ya vitabu 3,000 au 4,000 pekee,” alieleza kwa huzuni.

 Hazina ya Vitu vya Kale vya Kihistoria

Miongoni mwa vifusi, wajitolea waliokuwa na matumaini ya kurejesha mkusanyiko huo walichunguza vipande vilivyoteketea vya maandiko ya kale na karatasi zilizochakaa kwa muda.

“Maktaba ya Msikiti Mkuu wa Omari inachukuliwa kuwa maktaba ya tatu kwa ukubwa nchini Palestina, baada ya maktaba ya Msikiti wa AlAqsa na maktaba ya Ahmed Pasha alJazzar,” alisema AlAmsi.

Aliongeza kuwa ni maktaba muhimu ya kihistoria, yenye maandiko ya asili na mkusanyiko mpana wa vitabu katika nyanja za fiqhi, tiba, sheria ya Kiislamu, fasihi, na taaluma nyingine mbalimbali.

Historia ya Gaza inarejea maelfu ya miaka nyuma, na kuifanya ardhi hiyo kuwa hazina ya urithi wa kale, ikijumuisha athari za ustaarabu wa Wakanaani, Wamisri, Waajemi na Wagiriki.

Hata hivyo, zaidi ya miaka miwili ya vita imeacha athari kubwa kwa maeneo ya urithi wa kihistoria wa Gaza.

Kufikia Januari 2026, shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya utamaduni UNESCO lilithibitisha uharibifu wa maeneo 150 ya kihistoria, yakiwemo maeneo 14 ya kidini na majengo 115 yenye thamani ya kihistoria au kisanaa.

 “Ni Mashahidi wa Historia”

Ndani ya moja ya vyumba vya mawe vya zamani vya maktaba, mwanamke mmoja alionekana akitumia brashi ndogo kusafisha kitabu cha kale, huku wengine waliojitolea, wakiwa wamevaa barakoa na glovu, wakipitia rundo la vitabu vilivyoanguka chini.

“Hali ya vitabu vya nadra na vya kihistoria ni mbaya sana kwa sababu vimeachwa bila matunzo kwa zaidi ya siku 700 hadi 800,” alisema AlAmsi, akieleza kuwepo kwa “uharibifu mkubwa na mabaki ya baruti” juu ya maandiko hayo.

Tume huru ya Umoja wa Mataifa iliripoti mwezi Juni 2025 kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya shule, maeneo ya ibada na vituo vya kitamaduni huko Gaza yanachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita.

“Israel imeangamiza mfumo wa elimu wa Gaza na kuharibu zaidi ya nusu ya maeneo yote ya kidini na kitamaduni,” ilisema Tume ya Kimataifa ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ardhi Zinazokaliwa.

Utawala wa Israel ulipinga ripoti hiyo, ukiitaja kuwa ya “upendeleo na kisiasa”, na kudai kuwa ni jaribio jingine la “kusukuma simulizi ya kubuniwa kuhusu vita vya Gaza.”

Kwa AlAmsi, umuhimu wa kuokoa vitabu hivi unaenda zaidi ya karatasi na wino.

 “Vitabu hivi vinawakilisha historia ya mji wetu na ni mashahidi wa matukio ya kihistoria,” alisema.

3496556

Habari zinazohusiana
captcha