IQNA

Mahmoud Khalil apigana ajili ya uhuru wa kujieleza Marekani

17:44 - May 24, 2026
Habari ID: 3482279
IQNA – Mahmoud Khalil, mwanaharakati Mpalestina, amekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Marekani ili kuzuia kufukuzwa kwake nchini humo.

Hatua hii ni mwendelezo wa mzozo mkali wa kisheria dhidi ya utawala wa Trump. Uamuzi huu wa kuifikisha kesi hiyo katika ngazi ya juu zaidi ya mahakama nchini humo unakuja baada ya Mahakama ya Rufaa ya Mzunguko wa Tatu (Third Circuit Court of Appeals), katika uamuzi wa kura 6 kwa 5 uliotolewa Ijumaa, kutangaza kuwa haitafungua tena shauri la uamuzi uliotoa mwanya wa kufukuzwa kwa Khalil.

Brett Max Kaufman, mwanasheria mkuu katika Umoja wa Haki za Kiraia wa Marekani (ACLU), amesema katika taarifa yake: “Uamuzi wa Ijumaa siyo neno la mwisho, na bado tunaamini kikamilifu katika hoja zetu tunazoendelea nazo.”

Aliongeza kuwa: “Mahakama za shirikisho lazima ziwe na mamlaka ya kuingilia kati wakati serikali inapotumia vibaya mfumo wa uhamiaji wa nchi yetu ili kuwaadhibu watu kwa sababu ya matamshi yao yanayolindwa na Katiba. Ikiwa utawala wa Trump unaweza kumlenga, kumkamata, kumzuilia, na kumfukuza Mahmoud kwa sababu ya maoni yake, wanaweza kumfanyia hivyo yeyote anayetoa maoni wasiyokubaliana nayo.”

Wiki iliyopita, mawakili wa Khalil waliwasilisha rufaa nyingine tofauti dhidi ya amri ya Bodi ya Rufaa ya Uhamiaji (BIA) ya kutaka kumfukuza Khalil, wakiiomba mahakama kusitisha kesi hiyo kikamilifu. Rufaa hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Rufaa ya Mzunguko wa Tano, ikiitaka mahakama hiyo kubatilisha uamuzi huo kwa sababu hakimu katika kesi hiyo anadaiwa kukataa kuzingatia ushahidi muhimu.

Changamoto hiyo pia inadai kuwepo kwa utovu wa nidhamu wa hali ya juu katika kesi hiyo, ikiwemo madai ya maafisa wa serikali kuingilia kati mwenendo wa shauri hilo kwa kumshinikiza hakimu wa uhamiaji aliyesimamia kesi hiyo, iliyofanyika katika mahakama ya rufaa ya uhamiaji inayosimamiwa na Idara ya Sheria badala ya chombo huru cha mahakama.

Baher Azmy, Mkurugenzi wa Kisheria katika Kituo cha Haki za Kikatiba, alisema: “Tunatumai Mahakama Kuu itatambua jinsi uamuzi wa Mzunguko wa Tatu ulivyo na hatari, si tu kwa Mahmoud bali kwa wageni wengine ambao utawala unawalenga kwa kisasi.”

Khalil, ambaye ni msemaji wa maandamano ya kuunga mkono Gaza katika chuo kikuu na mkazi wa kisheria nchini Marekani, alikamatwa na Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Forodha ya Marekani (ICE) mnamo Machi 2025 na kuzuiliwa kwa siku 104. Baadaye, hakimu wa shirikisho alitangaza kuwa kuzuiliwa kwake kulikua kinyume cha katiba. Hata hivyo, utawala wa Trump ulishinda rufaa mapema mwezi Machi mwaka huu, hatua iliyoruhusu kesi hiyo kuendelea katika mahakama ya uhamiaji.

3497568

Habari zinazohusiana
captcha