Zoezi hili lilianza wiki kadhaa kabla ya kuanza kwa msimu wa Hija wa mwaka huu.
Zaidi ya kadi 150,000 tayari zimekwishatolewa hadi sasa. Kadi hizi zina taarifa muhimu kuhusu hujaji, kama vile maeneo ya makazi katika miji mitakatifu ya Makka na Madina na maeneo mengine matakatifu, pamoja na maelezo ya mawasiliano ya kampuni inayomhudumia hujaji husika.
Hili linasaidia katika kuwaongoza mahujaji kwa urahisi na kupunguza hatari ya mahujaji kupotea.
Aidha, kadi hizi hubeba taarifa za historia ya afya ya hujaji ikiwa ipo.
Mamlaka zimeeleza kuwa ni wajibu kwa kila hujaji kubeba kadi hii katika kipindi chote cha msimu wa Hija.
Uchapishaji wa kadi utaendelea hadi pale vibali vyote vya Hija na visa vitakapokamilika.
Kadi hizi zimechapishwa kwa viwango vya juu vya ubora na usalama, zikiwa na sifa maalum za kiusalama zinazozuia kughushi na kusaidia kuthibitisha hadhi halali ya hujaji.
Mahujaji kutoka nje ya Saudi Arabia hupokea kadi hizi wanapowasili, ilhali mahujaji wa ndani hupatiwa kadi hizo kupitia makampuni yanayowahudumia kabla ya kuanza kwa msimu wa Hija,
Wizara ya Hija na Umrah ya Saudi Arabia tayari imetangaza tarehe 29 Aprili kama mwisho wa mahujaji wote wa kigeni wa Hija ndogo ya Umrah kuondoka nchini humo, kwani maandalizi ya Hija ya mwaka huu yanashika kasi kuelekea mwezi Juni.
Wizara imesisitiza kuwa kukiuka tarehe hiyo ni kosa la kisheria linaloweza kusababisha adhabu kali.
Onyo hili limetolewa kutokana na wasiwasi wa baadhi ya wageni wa Umrah kubaki kinyume cha sheria kwa nia ya kushiriki ibada ya Hija bila idhini sahihi katika mji mtakatifu wa Makka na maeneo yanayozunguka.
Wizara imezitaka kampuni za Umrah na mahujaji kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni zilizowekwa kuhusu kuondoka kwa wakati uliopangwa.
3492844