
Kwa mujibu wa ripoti ya IQNA ikinukuu gazettengr, Bola Tinubu, Rais wa Nigeria, alitangaza mkakati wa kitaifa wa uchumi wa Halal wa nchi hiyo, unaolenga kuingia kikamilifu katika soko la Halal lenye thamani ya dola trilioni 8 za Marekani, sambamba na juhudi za kubadilisha na kupanua msingi wa uchumi wa taifa.
Katika hotuba yake ya kutangaza mkakati huo, Tinubu amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua zilizo na mpangilio na zinazojumuisha jamii zote, ili kuimarisha ajira na ustawi wa wananchi kote nchini. Amebainisha kuwa uzinduzi wa mkakati huu ni ishara ya utayari wa Nigeria kunyakua sehemu kubwa ya uchumi wa kimataifa wa Halal sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipewa kipaumbele na mataifa yaliyo mstari wa mbele.
Rais Tinubu alisema kuwa ifikapo mwaka 2027, inatarajiwa takribani dola bilioni 1.5 zitaongezeka katika Pato la Taifa (GDP) la Nigeria. “Kwa hisia hii ya uwajibikaji, ninazindua rasmi Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Halal wa Nigeria. Hati hii ni tamko la ahadi yetu ya kufikia viwango vya kimataifa kwa kuzingatia uwezo wa Nigeria, na kubadilisha fursa kuwa thamani ya kiuchumi endelevu,” alisema.
Aliendelea kusisitiza kuwa hatua za baadaye lazima ziwe za utaratibu na shirikishi, ili mkakati huu uwe chachu ya ajira, mauzo ya nje, na ustawi wa pamoja katika maeneo yote ya nchi.
Rais wa Nigeria alieleza kuwa kufikia mwaka 2030, mauzo ya nje ya vyakula vinavyozingatia sheria za Halal, pamoja na maendeleo ya minyororo ya thamani katika sekta ya dawa na vipodozi, yataifanya Nigeria ijitambulishe kama kitovu cha utalii unaoheshimu misingi ya Halal.
Habari inayohusiana:
Tinubu aliongeza kuwa mataifa yanayojihusisha na biashara ya Halal yanazidi kuzungumza na walaji, wawekezaji na washirika wa kibiashara wanaotafuta uhakika mkubwa kuhusu namna bidhaa zinavyozalishwa, kufadhiliwa na kusambazwa. “Nigeria sasa inajipanga na kujithibitisha ndani ya uelewa huu mpana,” alisema.
Akitaja nchi zilizoendelea kama Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Marekani, Kanada, Australia na New Zealand, Rais Tinubu alisema uzoefu wao unathibitisha ukweli mmoja wa msingi: uchumi wa Halal ni “soko la kimataifa linalojengwa juu ya viwango, usalama na imani ya mlaji, si jiografia wala imani ya kidini.”
Neno la Kiarabu, Halal linamaanisha bidhaa au huduma ambazo zinaruhusiwa kutumika kwa sababu zimetayarishwa kwa mujibu wa Sharia (sheria za Kiislamu).
4332846