
Mamlaka Kuu ya Huduma za Msikiti Mkuu wa Makka-Al Masjid Haram na Msikiti wa Mtume (SAW)-Al Masjid An Nabawi, imetangaza kukamilika kwa matengenezo ya kawaida ya Al‑Kaaba Tukufu na Hijr Ismail, kwa kuzingatia viwango vya juu kabisa vya kihandisi na kiufundi.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, mradi huo ulitekelezwa chini ya mpango madhubuti wa kiutendaji uliolenga kuhakikisha mtiririko mzuri wa mahujaji bila kuathiri utekelezaji wa ibada zao.
Kazi hizo zilihusisha takribani saa 4,700 za kazi ya wataalamu, na zilijumuisha vifurushi 31 vikuu vya kazi pamoja na shughuli 305 tofauti. Kazi hizo zilihusisha matengenezo ya sehemu za ndani za Al‑Kaaba, paa lake na maeneo yanayoizunguka, pamoja na ukaguzi na majaribio ya kina.
Aidha, kazi hizo zilijumuisha kubadilishwa kwa zaidi ya mita 30 za viungio vya upanuzi (silicone) vinavyoizunguka Al‑Kaaba, kujaza upya zaidi ya mita 50 za viungio vya marumaru, pamoja na kung’arisha na kukamilisha sakafu za marumaru zinazozunguka Al‑Kaaba kutoka pande zote.
Mradi huo ulitekelezwa na wataalamu wazalendo wenye ujuzi, wakitumia teknolojia za kisasa na vifaa vinavyokidhi viwango vya kimataifa, jambo lililoongeza ufanisi wa uendeshaji na kuhakikisha uimara wa muda mrefu wa sehemu mbalimbali za Al‑Kaaba Tukufu.
3497137