IQNA

Msikiti Mkuu wa Makkah Kuandaa Kozi ya Kuhifadhi Qur’ani Tukufu

19:24 - June 06, 2026
Habari ID: 3482330
IQNA – Usajili umeanza kwa wale wanaotaka kushiriki kozi ya majira ya kiangazi ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu katika Msikiti Mkuu wa Makkah (Masjid Al-Haram).

Urais Mkuu wa Masuala ya Msikiti Mkuu na Msikiti wa Mtume (SAW) umetangaza kuanza kwa usajili wa darsa hiyo ya majira ya kiangazi ya kuhifadhi Qur’ani kwa mwaka 1448 Hijria, kwa mujibu wa Shahid Al‑Alan.

Lengo la kozi hii ni kuimarisha kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kuweka misingi madhubuti ya usomaji (tilawah), hifdh (kuhifadhi) na muraja’ah (mapitio) miongoni mwa washiriki, kupitia programu maalumu na zilizoandaliwa kwa urahisi, chini ya usimamizi wa walimu na walimah wabobezi.

Kozi hii inajumuisha vipengele vitatu vikuu: kuhifadhi, kurejea (mapitio), na usomaji wa Qur’ani, na usajili uko wazi kwa wanaume na wanawake.

Washiriki pia watapatiwa cheti cha kuhitimu kozi hiyo.

Aidha, programu hii itatoa fursa ya kujifunza qira’aat mbalimbali za Qur’ani Tukufu.

Kwa mujibu wa Urais huo, kozi itafanyika kuanzia tarehe 13 Muharram hadi 16 Safar 1448 Hijria, kila siku kuanzia saa 12 alfajiri hadi saa 5 asubuhi, ndani ya Msikiti Mkuu wa Makkah.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi za kupanua mafundisho ya Qur’ani Tukufu, kuimarisha halaqah za Qur’ani na usomaji wake, pamoja na kuwapa mahujaji na waumini fursa ya kuungana kwa karibu zaidi na Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa njia ya kuhifadhi, kusoma na kufanya mapitio, na hivyo kuutajirisha uzoefu wao wa kiroho na kielimu katika Msikiti Mkuu.

4356516

captcha