IQNA

Kisomo cha Qur’an kabla ya penalti na sijda baada ya mechi vya timu ya Morocco

12:52 - July 01, 2026
Habari ID: 3482425
IQNA – Kisomo cha aya za Qur’an kilichofanywa na timu ya taifa ya Morocco kabla ya mikwaju ya penalti pamoja na sijda zao za shukrani baada ya ushindi dhidi ya Uholanzi katika hatua ya 32 Bora kimeenea kwa kasi katika mitandao ya kijamii duniani.

Video zinazoonyesha matukio hayo ya kidini zimepokelewa kwa mwamko mkubwa katika majukwaa mbalimbali ya mtandaoni.

Dakika chache kabla ya mikwaju ya penalti yenye presha kubwa kuanza, wachezaji wa Morocco pamoja na benchi la ufundi wakiongozwa na kocha mkuu Mohamed Ouahbi walikusanyika kwa duara, wakasoma aya za Qur’an Tukufu na kisha kuomba dua.

Mandhari hiyo ilisambaa sana mtandaoni baada ya Morocco kuibuka na ushindi wa penalti 3-2 dhidi ya Uholanzi kufuatia sare ya 1-1, na hivyo kufuzu kwenda hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia 2026.

Baada ya Ismael Saibari kufunga penalti ya ushindi, wachezaji pamoja na benchi la ufundi walisherehekea kwa kufanya sijda ya pamoja ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kabla ya kukumbatiana kwa furaha.

Hatua hiyo ilisifiwa sana na mashabiki duniani, ingawa si jambo jipya kwa “Atlas Lions”. Kwa miaka kadhaa sasa, timu ya taifa ya Morocco imekuwa ikijulikana kwa kuswali kabla ya mechi muhimu na kufanya sijda baada ya michezo, iwe ni ushindi au hata matokeo yasiyoridhisha.

Miongoni mwa wachezaji waliowahi kuzungumzia wazi umuhimu wa imani katika maisha yao ni beki wa Manchester United, Noussair Mazraoui. Nyota huyo wa Morocco amewahi kusema kuwa Uislamu una nafasi kuu katika maisha yake, huku pia akieleza azma yake ya kuhifadhi Qur’an Tukufu. Aidha, amesema anatamani kuendeleza masomo ya dini na kuitumikia jamii yake baada ya kustaafu soka.

Mazraoui alikuwa tena miongoni mwa wachezaji waliotoa kiwango bora dhidi ya Uholanzi, akiisaidia Morocco kubaki imara safu ya ulinzi kabla ya kipa Yassine Bounou kuokoa penalti muhimu katika mikwaju ya maamuzi, huku Saibari akifunga penalti ya ushindi.

Saibari, ambaye hivi karibuni amejiunga na Bayern Munich, ameibuka kuwa mmoja wa nyota muhimu wa Morocco katika mashindano hayo. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 tayari amefunga mabao matatu katika mechi nne, akitikisa nyavu katika michezo yote mitatu ya hatua ya makundi kabla ya kufunga penalti ya ushindi dhidi ya Uholanzi kwa utulivu mkubwa.

Sasa Morocco itachuana na Canada katika hatua ya 16 Bora huku ikiendeleza kampeni yake iliyovutia wengi katika Kombe la Dunia la FIFA 2026.

3498047

captcha