IQNA

Mwandishi wa Iraq: Ushiriki wa Mamilioni katika Mazishi ya Kiongozi Shahidi una ujumbe wenye nguvu

16:56 - July 14, 2026
Habari ID: 3482483
Rahbar Iraq
IQNA – Uwepo wa mamilioni ya waumini katika misafara ya mazishi iliyofanyika nchini Iran na Iraq kwa ajili ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyed Ali Khamenei, unabeba ujumbe muhimu, wa kina na wenye nguvu.

Haya yamesemwa na mwandishi na mwanaharakati wa vyombo vya habari wa Iraq, Adel Al‑Jabouri, ambaye aliandika katika makala kwamba ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump alishangazwa na mamilioni ya watu waliomiminika katika mitaa ya Tehran na miji mingine ya Iran kuomboleza na kumuaga Kiongozi wao, basi huenda alishangazwa zaidi na kubaki bumbuwazi alipoona mamilioni ya Wairaq waliyojaa mitaani wakipaza sauti kaulimbiu za “Mauti kwa Marekani na Israel”.

Makala ya Al‑Jabouri ni kama ifuatavyo:

Kama ilivyokuwa nchini Iran, mamilioni ya Wairaq kutoka sehemu mbalimbali za nchi walishiriki katika mazishi ya kihistoria na yasiyo na mfano ya Ayatullah Seyed Ali Khamenei katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala. Vyanzo mbalimbali vimekadiria idadi ya washiriki katika mazishi hayo katika miji hiyo miwili kufikia karibu watu milioni kumi. Hii ni idadi kubwa sana, lakini kwa yeyote anayefahamu, kuelewa na kuthamini uhusiano, mafungamano na mambo ya pamoja yanayowaunganisha watu wa Iraq na Iran, pamoja na misimamo ya heshima iliyochukuliwa na uongozi wa Iran katika kuisaidia Iraq katika nyakati zake ngumu zaidi, jambo hili si la kushangaza wala la ajabu.

Mahudhurio haya makubwa ya mamilioni ya watu, yaliyoandamana na taswira za kugusa hisia na ubinadamu, yanabeba ujumbe muhimu, wa kina na wenye nguvu. Miongoni mwa ujumbe huo, uliojitokeza zaidi ni huu:

Kwanza: Watu wa Iraq huendelea kuwa waaminifu kwa wale wanaosimama pamoja nao, wanaowaunga mkono na kuwatetea wanapohitaji msaada. Bila shaka, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran , yaani Kiongozi wake Mkuu, taasisi za serikali, wasomi wa kisiasa na kijamii, pamoja na wananchi wake kwa ujumla, ilikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa zaidi wa watu wa Iraq wa makundi yote na mielekeo yote katika kipindi walipokuwa wakijitahidi kujikomboa kutoka katika utawala wa kidikteta na wa umwagaji damu wa Chama cha Baath.

Baadaye, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisimama mstari wa mbele katika kuisaidia Iraq na watu wake kujenga mfumo wao mpya wa kidemokrasia baada ya kuanguka kwa utawala wa Baath wa Saddam Hussein katika majira ya kuchipua ya mwaka 2003. Vilevile ilisimama pamoja nao katika kukabiliana na ugaidi wa kitakfiri wa Al‑Qaeda na baadaye Daesh (ISIS), ambao uliundwa na baadhi ya madola ya kikanda na kimataifa yakiongozwa na Marekani kwa lengo la kuitumbukiza Iraq katika migogoro ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi na kuirudisha nyuma badala ya kuisukuma mbele.

Pili: Iraq imekuwa, ipo na itaendelea kuwa mwanachama imara na hai wa Muqawama (Mhimili wa Mapambano ya Kiislamu). Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni na washirika wengine waliweka matumaini yao katika kuanguka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kumlenga Kiongozi wa Mapinduzi na viongozi waandamizi wa mfumo huo, huku wakijaribu wakati huohuo kuudhoofisha, kuutenga na kuuzingira Muqawama, hasa makundi yaliyo karibu zaidi na Iran. Hata hivyo, matukio yameonyesha upuuzi na kutokuwa na msingi kwa makadirio hayo. Mfumo wa Iran haukuanguka baada ya kuuawa shahidi kwa Kiongozi wake, wala vikosi vya Muqawama havikusalimu amri.

Iwapo tutaweka kando misimamo yote ya awali na kuangazia tu mazishi yaliyohudhuriwa na idadi isiyo ya kawaida ya Wairaq, hilo pekee linatosha kuwa ushahidi ulio wazi zaidi kwamba Iraq bado iko katikati ya Muqawama na inashikamana imara na misingi na misimamo yake.

Ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump alishangazwa na mamilioni ya watu waliomiminika katika mitaa ya Tehran na miji mingine ya Iran kuomboleza na kumuaga Kiongozi wao, basi huenda alishangazwa zaidi alipoona mamilioni ya Wairaq wakijaza mitaa, wakikusanyika kuzunguka jeneza la Kiongozi Shahidi na wakipaza sauti kaulimbiu za “Mauti kwa Marekani”, “Mauti kwa Israel”, na hata “Mauti kwa Trump”.

Tatu: Ikiwa kulikuwa na watu huko Tel Aviv, Washington na maeneo mengine waliokuwa na matumaini ya kuiingiza Iraq katika mkondo wa kuanzisha mahusiano na utawala wa Kizayuni kupitia misamiati na majina yenye kupotosha kama vile “Makubaliano ya Ibrahim”, “Mashariki ya Kati Mpya” au “Mpango wa Karne”, basi mazishi ya Ayatullah Seyed Ali Khamenei yaliyohudhuriwa na mamilioni ya watu yalivunja matumaini hayo yote.

Mazishi hayo yalithibitisha kwamba amani inayotafutwa na Marekani na utawala wa Kizayuni si chochote ila ndoto isiyoweza kutekelezeka. Amani ya kweli haitapatikana kupitia mikutano ya faragha au kusainiwa kwa nyaraka zilizoandaliwa na akili zenye nia mbaya na zilizoshindwa. Badala yake, itapatikana kupitia matakwa ya mataifa na wananchi wanaopigania kurejesha haki zao zilizoporwa, kupotezwa na kunyang’anywa, pamoja na msaada na uungaji mkono wa mataifa na watu wanaosimama pamoja nao kwa njia zote zinazowezekana.

Kama makubaliano ya udhalilishaji yangekuwa ndiyo yanayoamua hatima ya mambo, basi mapambano ya watu wa Palestina, watu wa Lebanon na mataifa mengine yasingeendelea, wala utawala wa Kizayuni usingekumbwa na misururu ya kushindwa na kuishi katika hofu ya kudumu ya kudhoofika na kuporomoka.

Nne: Wanaounda uhalisia wa matukio, wanaobainisha mielekeo, wanaochora njia za kusonga mbele na wenye kauli ya mwisho katika medani ni mataifa na wananchi, si tawala na serikali. Kwa msingi huo, Wairaq hao mamilioni waliolibeba jeneza la Kiongozi Shahidi katika nyoyo na nafsi zao na kuliinua juu ya mikono na mabega yao hawakuchukua msimamo mpya, bali walithibitisha, waliimarisha na walizidisha kushikamana kwao na misimamo, misingi, itikadi na mielekeo yao ya awali. Hakuna aliyeweza kuwazuia kufanya hivyo.

Hao Mamilioni waliojitokeza ni wale ambao kila mwaka huhuisha ahadi ya kujitolea, utiifu na uaminifu kwa Sayyid al‑Shuhada, Imam Hussein (AS), katika siku ya Ashura na Arubaini. Nao ndio hao hao waliokabiliana na dhulma, ukandamizaji na uonevu wa utawala wa Baath uliotoweka, na ndio hao hao waliowashinda magaidi wa Al‑Qaeda na Daesh na kuvuruga njama na mipango ya Marekani pamoja na utawala vamizi wa Kizayuni.

3498236

Habari zinazohusiana
captcha