
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein aliyekuwa ziarani Tehran siku ya Jumapili, Araghchi alibainisha kuwa mamilioni ya Wairani husafiri kwenda Iraq kutembelea maeneo matukufu katika nyakati mbalimbali, hususan katika mwezi wa Muharram na wakati wa matembezi ya Arbaeen.
Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa Kishia siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, likikumbusha kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu katika madhehebu ya Shia.
Ni miongoni mwa hija kubwa zaidi duniani zinazofanyika kila mwaka, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia, pamoja na baadhi ya Waislamu wa Sunni na wafuasi wa dini nyingine, hupanda na kutembea kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekaribisha kukabidhiwa kambi ya anga ya Ain al Asad kwa vikosi vya jeshi la Iraq na kuitaja hatua hiyo kuwa ishara ya kuimarishwa utuvulivu na mamlaka ya kujitawala Iraq.
Araqchi amemshukuru Fuad Hussein kwa ziara yake nchini na kusema pande mbili tayari zimefanya duru mbili za majadiliano yaliyozaa matunda.
Amesisitiza kuwa kukabidhiwa kwa Iraq kambi ya anga iliyokuwa ikidhibitiwa na Marekani ni hatua iliyoungwa mkono pakubwa na Jamhuri ya Kiislamu.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran kwa mara nyingine tena amethibitisha nia thabiti ya Tehran ya kuiona Iraq ikiwa imara, inayojitawala na yenye muundo huru wa kisiasa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria uhusiano unaozidi kuimarika kati ya mataifa hayo mawili na kueleza kuwa makumi ya maelfu ya wanafunzi wa Iraq wanasoma nchini Iran, na zaidi ya raia milioni saba husafiri kati ya nchi hizo mbili kila mwaka.
Araqchi ameongeza kuwa yeye na mwenzake wa Iraq wamejadili mapendekezo ambayo yanaweza kuratibiwa kidiplomasia kati ya Iran na Iraq ili kuboresha amani na utulivu katika kanda hii.
3496098