IQNA

Kiongozi wa Yemen: Marekani na Israel zinahasimiana na Iran kwa sababu inazuia njama zao

6:38 - February 14, 2026
Habari ID: 3481932
IQNA-Kiongozi wa harakati ya Muqawama (mapambano ya Kiislamu) ya Ansarullah nchini Yemen amesema kuwa Marekani na Utawala wa Israel zinakabiliana na Iran kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasimama kama kizuizi dhidi ya mradi wao mpana wa kutawala eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati.

Akizungumza siku ya Ijumaa, Sayyid Abdul-Malik Badr al-Din al-Houthi alisema kuwa: “Adui wa Kizayuni, kwa kushirikiana na Marekani, analenga kuyatawala mataifa ya eneo hili,” akisisitiza kuwa sababu kuu ya kulengwa kwa Iran ni nafasi yake ya kuzuia na kudhoofisha njama hizo. Aliitaja misimamo ya Iran kuwa “imara na thabiti,” akiielezea Tehran kama ngome imara inayokwamisha ajenda ya pamoja ya Marekani na Israel.

Kauli hizo zimekuja huku kukishuhudiwa ongezeko la vitisho vya Marekani dhidi ya Iran, huku Rais wa Marekani Donald Trump akiendelea kutuma meli za kivita na vikosi vingine katika maeneo yaliyo karibu na Iran, sambamba na kuendelea kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Washington na Tehran kuhusu suala la nyuklia. 

Al-Houthi amesema kuwa Umma wa Kiislamu kwa ujumla unakabiliwa na mashinikizo yanayoongezeka. “Umma unakumbwa na changamoto, na kuna matatizo mengi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu,” alisema, akionya kuwa changamoto hizo zinaibuka kwa wakati mmoja. Ameongeza kuwa makabiliano hayo hayapo tu katika uwanja wa kijeshi au kisiasa. “Maadui, kupitia vita laini (soft war), wanajaribu kuukata uhusiano wa Umma na uongofu wa Mwenyezi Mungu na Uislamu, ili kusiwe na mshikamano wa kujikinga,” amesema. “Leo tunakabiliwa na vita vikubwa zaidi vya fikra tangu mwanzo wa jamii ya binadamu,” ameongeza, akielezea mapambano hayo kuwa ya kiitikadi pamoja na ya kijiografia na kisiasa. Kiongozi huyo wa Yemen pia amekosoa hali ya kutojali inayosambaa katika mataifa ya Kiislamu. Amesema kuwa watu wengi wanapuuza hatari zinazoukabili Umma, lakini akaonya kuwa “uzembe huo hauna manufaa.” Amesisitiza kuwa kujitenga na wajibu na kubaki bila ufahamu wa uhalisia ni jambo “hatari.”

Ameendelea kusema kuwa Umma unakabiliwa na vitisho kutoka kwa “maadui wenye chuki, yaani Uzayuni, pamoja na matawi yake ya Kimarekani, Kizayuni cha Israel na Uingereza.” Kwa mujibu wa kiongozi wa Ansarullah, matukio ya kikanda yamefikia “hatua ya maamuzi,” huku juhudi za kulazimisha mlinganyo wa upande mmoja juu ya Umma zikichukuliwa, mwelekeo aliouelezea kuwa “hatari sana.” Kiongozi huyo wa Yemen amebaini kuwa utawala wa Israel unatekeleza makosa na uhalifu mbalimbali dhidi ya wananchi wa Palestina, Lebanon, na Syria, akisisitiza kuwa matukio ya eneo hilo yanapaswa kuangaliwa ndani ya muktadha wa sera za kuutwisha Umma, zinazotokana na misimamo ya Kimarekani-Kizayuni.

Aidha, amesema kuwa Israel inalenga kufuta urithi wa Kiislamu katika maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kwa kubomoa maeneo ya kihistoria na kuwafukuza wakazi wake. Amesema pia kuwa utawala huo unafanya kazi ya kulinyakua rasmi eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kukomesha uwepo wa Wapalestina huko, huku ukipuuza waziwazi makubaliano yote yaliyopo, yakiwemo Mikataba ya Oslo na yaliyoifuata. Aidha, amebainisha kuwa Israel imepanua uhuru kwa walowezi wenye silaha, sambamba na kuongezeka kwa mashambulizi ya walowezi dhidi ya Wapalestina katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Habari inayohusiana:

Kuhusu Gaza, al-Houthi amesema kuwa Israel inaendelea na mauaji huku ikiendeleza mzingiro mkali ulioufanya maisha ya kila siku kuwa magumu kupindukia. Amesisitiza kuwa mateso ya watu wa Gaza walioko chini ya mzingiro ni makubwa na ya kuumiza.

Ikumbukwe kuwa Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023, na hadi wakati huo, jeshi katili la utawala huo limeua zaidi ya Wapalestina 72,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Mauaji hayo yameendelea licha ya kusitishwa kwa mapigano kulikosimamiwa na Marekani, ambapo utekelezaji ulianza Oktoba mwaka jana. Utawala wa Israel umekataa kutimiza kikamilifu ahadi zake chini ya makubaliano hayo, ikiwemo kufungua vivuko kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

4334267

captcha