
Chuo Kikuu cha Al-Kafeel University katika mji mtakatifu wa Najaf, Iraq, kiliandaa kongamano hilo la kielimu siku ya Jumatano na Alhamisi, Februari 11–12, 2026.
Mkutano huo uliandaliwa chini ya kaulimbiu: “Urithi wa Sheikh Tusi katika Fikra za Kiislamu na Kimagharibi; Mitazamo ya Kisasa”, kwa udhamini wa Taasisi ya Usimamizi wa Haram Tukufu ya Hadhrat Abbas (AS), na kwa ushiriki wa watafiti na wabobezi kutoka ndani na nje ya Iraq.
Kituo cha Tafiti na Utafiti wa Sheikh Tusi, kinachohusishwa na Kamati Kuu ya Uhuishaji wa Turathi ya taasisi hiyo, pamoja na Chuo Kikuu cha Al-Kafeel na Taasisi ya Utafiti wa Kishia ya Toronto, Canada, vilishiriki katika maandalizi ya kongamano hilo.
Kaulimbiu ya mkutano ilikuwa: “Hawza ya Najaf: Miaka Elfu ya Utoaji wa Kielimu”, ikiwa na lengo la kuadhimisha miaka elfu tangu kuasisiwa kwa hawza hiyo, na kuangazia utu wa pande zote wa Sheikh Tusi, ambaye aliweka misingi ya elimu za fiqhi, usul al-fiqh na tafsiri.
Sheikh Muhammad Hussein Bahsoun Ameli, mjumbe wa kamati ya maandalizi, alieleza kuwa Hawza ya Najaf ina nafasi adhimu kama moja ya vituo vya kale zaidi, vilivyo na mizizi imara na mwendelezo thabiti wa kielimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Aliongeza kuwa, kwa mnasaba wa kutimia milenia ya hijra ya Sheikh Tusi kutoka Baghdad kwenda Najaf, ilionekana kuwa ni wajibu wa kielimu kumhuisha mwanazuoni huyo kwa kuandaa mkutano wa kimataifa.
Alibainisha kuwa Kituo cha Sheikh Tusi kimebeba jukumu la kuhuisha turathi hiyo kupitia mradi mpana wa kisayansi unaolenga kufufua urithi wake na kuchambua maandiko yaliyotungwa kuhusu kazi zake.
Mapendekezo ya Mkutano
Mwisho wa shughuli za kongamano, kamati ya maandalizi ilitoa mapendekezo yafuatayo:
1. Kuongeza juhudi za kisayansi, kuunganisha uwezo na kukusanya nguvu za utafiti kutoka taasisi na vituo mbalimbali vya kielimu kwa lengo la kuhudumia urithi wa Hawza ya Najaf na wanazuoni wake wakubwa.
2. Kuitambulisha Hawza ya Najaf na shakhsia zake katika kipindi cha miaka elfu ya utoaji endelevu wa kielimu.
3. Kuangazia nafasi ya Hawza ya Najaf kama mji mkuu wa kielimu wenye mizizi ya kina, ambao licha ya eneo lake dogo la kijiografia, umelea maelfu ya wanazuoni na shakhsia mashuhuri waliotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa ustaarabu wa Kiislamu katika nyanja za elimu, vitendo, harakati, siasa na jamii , sawa na vituo vikubwa vya elimu ya Kiislamu kama Al-Azhar nchini Misri, Al-Zaytouna nchini Tunisia, na Quaraouiyine nchini Morocco.
4. Kuhamasisha tafiti linganishi zinazoonesha athari ya Sheikh Tusi na Hawza ya Najaf kwa madhehebu mengine ya fiqhi na kalamu ya Kiislamu, na kufafanua namna athari hiyo ilivyosambaa Mashariki na Magharibi.
5. Kujitahidi kuanzisha hifadhidata ya kisayansi ya kidijitali inayojumuisha turathi za Sheikh Tusi na Hawza ya Najaf, zikiwemo nakala za maandishi ya kale, machapisho, tafiti na tasnifu za kitaaluma, ili kurahisisha upatikanaji wake kwa watafiti wa kimataifa.
6. Kuwasaidia watafiti chipukizi na wanafunzi wa shahada za juu, na kuwahamasisha kuchagua mada zinazohusiana na urithi wa Sheikh Tusi na Hawza ya Najaf.
7. Kusisitiza umuhimu wa kutafsiri tafiti thabiti zinazohusiana na Sheikh Tusi na Hawza ya Najaf katika lugha za kisasa, hususan Kiingereza na Kifaransa, ili kuimarisha uwepo wa kimataifa wa turathi hiyo.
8. Kuendelea kuandaa mikutano na semina za kisayansi za mara kwa mara kama jukwaa la majadiliano ya kielimu, kubadilishana uzoefu miongoni mwa watafiti, na kukuza hazina ya maarifa kuhusu historia ya Hawza ya Najaf na shakhsia zake.
Kwa jumla, mkutano huu umeashiria hatua mpya katika kuhuisha turathi za Najaf , kwa mtazamo unaounganisha heshima ya urithi wa kale na mahitaji ya zama za sasa, katika mizani ya elimu, tafakkuri na uwajibikaji wa kijamii.
*Inafaa kuashirikia hapa kuwa, Hawza (Kiarabu: حوزة), au ḥawzah ʿilmīyah (Kiarabu: حوزة علمیة), ni istilahi ya pamoja (wingi wake: hawzāt) inayotumika kumaanisha madrasa , yaani seminari au chuo cha juu cha Kiislamu— ambamo wanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Kishia hupata elimu na mafunzo ya juu ya kielimu na kiroho.
4334182