
Hapa chini ni matini kamili ya taarifa hiyo.
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Tunaujulisha umma mtukufu, mkubwa na mashujaa wa Iran kwamba adui katika vita vyake visivyo vya haki, visivyo halali na vya uhalifu dhidi ya taifa la Iran amepata kushindwa kwa namna isiyoweza kukanushwa, kushindwa kwa kihistoria na lenye athari kubwa. Kwa baraka za damu safi ya kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Imam Khamenei (Mwenyezi Mungu Amrehemu), pamoja na uongozi na maelekezo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), na kwa juhudi na ushujaa wa wapiganaji wa Uislamu katika medani za mapambano, hasa kutokana na uwepo wenu wa kihistoria, wa kudumu na wa kishujaa, enyi wananchi wapendwa, tangu siku za mwanzo kabisa za vita, Iran imepata ushindi mkubwa.
Kutokana na hali hiyo, Marekani imelazimika kukubali mpango wa vipengele kumi uliowasilishwa na Iran, ambao kimsingi unajumuisha kufungamana na kutofanya uchokozi dhidi ya Iran, kuendelea kwa udhibiti wa Iran juu ya Lango Bahari la Hormuz, kukubaliwa kwa haki ya Iran ya kurutubisha madini ya urani ya viwanda vya nyuklia, kuondolewa kwa vikwazo vyote vya msingi na vya pili vilivyowekwa dhidi ya Iran, kusitishwa kwa maazimio yote ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Bodi ya Magavana wa IAEA kulipwa fidia kwa Iran, kuondolewa kwa majeshi ya Marekani kutoka eneo la Asia Magharibi, pamoja na kusitishwa kwa vita katika nyanja zote, ikiwemo vita dhidi ya Harakati ya Muqawama ya Kiislamu ya Lebanon.
Tunawaponge wananchi wote wa Iran kwa ushindi huu na kusisitiza kwamba hadi maelezo ya mwisho ya ushindi huu yatakapokamilishwa, bado kunahitajika subira, busara ya viongozi na kudumishwa kwa umoja pamoja na mshikamano wa wananchi wa Iran.
Katika siku arobaini zilizopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na wapiganaji shujaa wa Muqawama huko Lebanon, Iraq, Yemen na Palestina inayokaliwa kwa mabavu wamempiga adui mapigo ambayo kumbukumbu ya kihistoria ya dunia haitayasahau kamwe. Iran na mhimili wa Muqawama, ambao ni wawakilishi wa heshima na utu wa kibinadamu mbele ya maadui walio wakatili zaidi dhidi ya ubinadamu, baada ya mapambano ya kihistoria wamewapa maadui hao somo lisilosahaulika. Katika mapambano hayo wameyavunja vibaya majeshi ya maadui, uwezo wao wa kijeshi, miundombinu yao, na hata mtaji wao wote wa kisiasa, kiuchumi, kiteknolojia na kijeshi, kiasi kwamba maadui sasa wako katika katika hali ya kudhoofika na kukata tamaa, bila kuona njia nyingine isipokuwa kukubali matakwa ya taifa kubwa la Iran na mhimili wenye heshima wa Muqawama.
Siku ya kwanza kabisa ambapo maadui wahalifu wa Iran walipoanzisha vita hivi vya dhuluma, walidhani kwamba ndani ya muda mfupi wangeweza kuiweka Iran chini ya udhibiti kamili wa kijeshi na, kwa kuzusha hali ya kutokuwa na utulivu wa kisiasa na kijamii, wangeilazimisha Iran kujisalimisha.
Walidhani kwamba mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran yangenyamazishwa kwa haraka, na hawakuamini kuwa Iran ingeweza kutoa jibu lenye nguvu kiasi hicho nje ya mipaka yake na katika upana wa eneo lote la kanda. Uzayuni mwovu wa kimataifa ulimshawishi rais asiye na busara wa Marekani kwamba vita hivi vingemaliza kabisa uwezo wa Iran, na kwamba kwa kuiondoa ngome hii ya mwisho ya utu na ubinadamu wangeweza baada ya hapo kutenda uhalifu wowote dhidi ya yeyote watakayemtaka bila kizuizi.
Walikuwa wakiiota ndoto ya kuigawa Iran tukufu vipande vipande, kupora mafuta na utajiri wake, na hatimaye kuwaacha Wairani wakiogelea katika hali ya machafuko, kutokuwa na utulivu na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi ijayo.
Wapiganaji jasiri wa Uislamu pamoja na washirika wao wenye ujasiri katika mhimili wa Muqawama, licha ya kwamba nyoyo zao zilikuwa zimejeruhiwa na kusononeshwa na shahada ya kiongozi wao, waliamua kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa kufuata mfano wa Bwana na Kiongozi wa mashahidi, kuwapa maadui hawa somo la kihistoria mara moja na ya mwisho. Walidhamiria kulipiza kisasi kwa uhalifu wote wa zamani walioufanya maadui, na kuunda hali ambayo itamlazimisha adui kuacha kabisa wazo la kuivamia Iran tukufu, na hatimaye aonje kikamilifu ladha ya fedheha na udhalili mbele ya taifa kubwa la Iran.
Kwa mkakati huo na kwa kutegemea umoja wa kisiasa na kijamii usio na mfano uliokuwa umejitokeza ndani ya nchi, Iran pamoja na Muqawama walianzisha moja ya mapambano mazito zaidi ya vita mseto katika historia dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni. Katika kipindi hiki waliweza kufikia malengo yote waliyokuwa wamepanga katika mapambano hayo. Iran na Muqawama waliuangamiza karibu kabisa mtambo wa kijeshi wa Marekani katika eneo, na wakatoa mapigo mazito na ya kina dhidi ya miundombinu na uwezo mkubwa ambao adui alikuwa ameujenga kwa miaka mingi katika eneo kwa ajili ya vita dhidi ya Iran na kuizingira.
Katika kiwango cha kikanda, walilisababishia jeshi la kihalifu la Marekani kupata hasara kubwa za wanajeshi. Ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) adui amepata mapigo makubwa na ya kumvunja nguvu kwa kulengwa majeshi yake , miundombinu, vifaa na mali zake. Wanamuqawama pia waliifanya pia hali kuwa ngumu kwa adui katika nyanja zote za mapambano kwa kiwango ambacho si tu kwamba hakuna hata moja ya malengo yake makuu yaliyotimia, bali pia maadui, takribani siku kumi tu baada ya kuanza kwa vita, walitambua wazi kwamba hawana kabisa uwezo wa kushinda vita hivi. Kwa sababu hiyo walianza kupitia njia na mifumo mbalimbali kujaribu kuwasiliana na Iran na kuomba kusitishwa kwa mapigano.
Taifa tukufu la Iran linapaswa kujua kwamba kwa baraka za juhudi za kujitolea za wana wao na kwa uwepo wao wa kihistoria katika medani, adui kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa amekuwa akiomba kwa msisitizo kusitishwa kwa mashambulizi makali ya Iran na Muqawama. Hata hivyo, viongozi wa nchi walikataa maombi hayo yote kwa sababu tangu mwanzo iliamuliwa kwamba vita vitaendelea hadi malengo yake yatimie, ikiwemo kumfanya adui ajutie na kufika katika hali ya kukata tamaa, pamoja na kuondoa tishio la muda mrefu dhidi ya Iran. Kwa sababu hiyo mapigano yaliendelea hadi leo, siku ya arobaini. Vilevile Iran hadi sasa imekataa mara kadhaa makataa yaliyotolewa na rais wa Marekani, na imeendelea kusisitiza kwamba haitoi umuhimu wowote kwa aina yoyote ya vitisho au muda wa mwisho unaowekwa na adui.
Sasa tunaliletea taifa kubwa la Iran bishara kwamba karibu malengo yote ya vita yamefikiwa, na wana wenu mashujaa wamemfikisha adui katika hali ya udhaifu wa kihistoria na kushindwa ambako kutabaki katika kumbukumbu kwa muda mrefu. Uamuzi wa kihistoria wa Iran, unaoungwa mkono kwa umoja na taifa zima, ni kuendeleza mapambano haya kwa muda wowote utakaohitajika hadi mafanikio yake makubwa yadhibitiwe kikamilifu na mpaka mizania mipya ya usalama na siasa katika eneo la kanda iundwe kwa msingi wa kukubalika kwa nguvu na uongozi wa Iran pamoja na Muqawama.
Katika muktadha huo, kwa mujibu wa uongozi na busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), na kwa idhini ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, pamoja na kuzingatia nafasi ya juu ambayo Iran na Muqawama wanayo katika uwanja wa mapambano na kushindwa kwa adui kutekeleza vitisho vyake licha ya madai yake yote, na pia kukubaliwa rasmi kwa matakwa halali ya wananchi wa Iran, imeamuliwa kwamba ili kukamilisha maelezo ya mwisho ya makubaliano, mazungumzo yafanyike Islamabad. Lengo ni kwamba ndani ya muda usiozidi siku kumi na tano, baada ya kukamilishwa kwa mapatano, ushindi wa Iran uliopatikana katika uwanja wa mapambano uthibitishwe pia katika uwanja wa mazungumzo ya kidiplomasia.
Katika muktadha huo, Iran ilikataa mapendekezo yote yaliyowasilishwa na upande wa adui na badala yake ikaandaa mpango wa vipengele kumi ambao uliwasilishwa kwa upande wa Marekani kupitia nchi ya Pakistan. Katika mpango huo, Iran ilisisitiza mambo ya msingi kama vile meli kupita katika Lango Bahari la Hormuz kwa usimamizi uratibu na majeshi ya Iran, jambo linaloipa Iran nafasi ya kipekee ya kiuchumi na kijiografia‑kisiasa, pamoja na ulazima wa kusitishwa kwa vita dhidi ya sehemu zote za mhimili wa Muqawama, jambo ambalo litamaanisha kushindwa kwa kihistoria kwa uchokozi wa utawala wa Israel unaoua watoto.
Mpango huo pia ulisisitiza kuondolewa kwa majeshi ya Marekani kutoka katika kambi na vituo vyote vya kijeshi vilivyopo katika eneo, kuanzishwa kwa itifaki maalumu ya usafiri salama katika Lango Bahari la Hormuz kwa namna itakayohakikisha udhibiti wa Iran kulingana na makubaliano ya itifaki hiyo, kulipwa kikamilifu kwa fidia ya hasara za Iran kulingana na tathmini zilizofanywa, kuondolewa kwa vikwazo vyote vya msingi na vya pili pamoja na maazimio ya Bodi ya Magavana ya IAEA na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuachiwa huru mali na rasilimali zote za Iran zilizozuiliwa nje ya nchi, na hatimaye kuidhinishwa kwa vipengele vyote hivi kupitia azimio la lazima la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Inafaa pia kubainishwa kwamba kupitishwa kwa azimio hilo kutayageuza makubaliano haya yote kuwa sheria ya kimataifa yenye nguvu ya lazima ya utekelezaji, jambo ambalo litahesabiwa kuwa ushindi muhimu wa kidiplomasia kwa taifa la Iran.
Sasa Waziri Mkuu wa Pakistan ameiarifu Iran kwamba upande wa Marekani, licha ya vitisho vyake vya nje na vya maneno, umekubali kanuni hizi kama msingi wa mazungumzo na hivyo kwa namna fulani umejikuta ukikubali matakwa ya taifa la Iran. Kwa msingi huo, katika ngazi ya juu kabisa imeamuliwa kwamba Iran kwa kipindi cha wiki mbili itafanya mazungumzo na upande wa Marekani mjini Islamabad, na mazungumzo hayo yatafanyika tu kwa kuzingatia kanuni hizi zilizowekwa.
Inasisitizwa kwamba hatua hii haimaanishi kumalizika kwa vita. Iran itakubali kumalizika kwa vita tu pale ambapo, kwa kuzingatia kukubaliwa kwa misingi iliyowekwa katika mpango wa vipengele kumi wa Iran, maelezo na vipengele vyake vyote vitakamilishwa na kuthibitishwa katika mazungumzo ya mwisho.
Mazungumzo haya, huku kukiwa na kutouamini upande wa Marekani, yataanza siku ya Ijumaa tarehe 10 Machi mjini Islamabad. Iran imetenga muda wa wiki mbili kwa ajili ya mazungumzo haya, na muda huo unaweza kuongezwa iwapo pande zote mbili zitakubaliana.
Katika kipindi hiki, ni muhimu kudumishwa umoja kamili wa kitaifa na sherehe za ushindi ziendelee kwa nguvu. Mazungumzo ya sasa yanachukuliwa kuwa mazungumzo ya kitaifa na mwendelezo wa mapambano katika uwanja wa vita. Kwa hiyo, inahitajika kwamba wananchi wote, wasomi na makundi ya kisiasa waamini mchakato huu unaoendeshwa chini ya uangalizi wa Kiongozi wa Mapinduzi na ngazi za juu kabisa za mfumo wa dola, na watoe uungwaji mkono wao. Vilevile wanapaswa kujiepusha kabisa na kauli au matamshi yoyote yanayoweza kuleta mgawanyiko.
Iwapo kushindwa kwa adui katika uwanja wa vita kutageuka kuwa mafanikio thabiti ya kisiasa katika mazungumzo, basi ushindi huu mkubwa wa kihistoria utaadhimishwa kwa pamoja. Lakini ikiwa hali haitakuwa hivyo, basi katika uwanja wa mapambano tutasimama bega kwa bega hadi kufikiwa kwa matakwa yote ya taifa la Iran. Mikono yetu bado iko juu ya vishindo vya silaha, na endapo adui atafanya kosa hata dogo, tutajibu kwa nguvu kamili.
Sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa
8 Aprili 2026
4345108