IQNA

Msahafu wa Najaf: Ushindi wa kishindo dhidi ya shaka za wapinzani wa Mashia

17:15 - May 24, 2026
Habari ID: 3482276
IQNA – Kwa miaka mingi, Iraq nzima, na hasa mji mtukufu wa Najaf, ilitegemea nakala za Qur’ani zilizochapishwa nje ya mipaka yake kwa ajili ya kusambazwa misikitini na katika vituo mbalimbali za kielimu.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, badala ya kutegemea nakala kutoka Beirut au Madina, mradi wa “Msahafu wa Najaf”, ulioanzishwa na Uongozi Mfawidhi wa Haram Takatifu ya Hazrat Abbas (A.S), umezinduliwa kama msahafu wa kwanza wenye utambulisho kamili wa Kiiraqi tangu hatua ya awali hadi kukamilika kwake.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Al-Kafeel, kwa miongo kadhaa, vyombo vya habari vyenye chuki vimekuwa vikijaribu kupanda mbegu za shaka kuhusu imani za Mashia au wafuasi wa Ahl-ul-Bayt (AS) kuelekea Qur’ani Tukufu kwa kupotosha ukweli. Pengine uongo mkubwa na wa mara kwa mara ni madai kwamba Waislamu Mashia wana Qur’ani yao tofauti na ile iliyo mikononi mwa Waislamu wengine; hilo ni jaribio duni la kutaka kuwatenga wafuasi wa shule ya Ahl-ul-Bayt (AS) na chanzo kikuu cha Uislamu.

Katika mazingira hayo, katika mji mtukufu wa Najaf na karibu na Haram ya Amirul-Mu’minin (AS), majibu ya kashfa hizi hayakutolewa kwa hotuba pekee, bali kupitia tukio la kihistoria, yaani uzinduzi wa Msahafu wa Najaf mnamo tarehe 29 Aprili 2026. Je, ni nini ukweli wa mafanikio haya? Je, mafanikio haya yatawafunga midomo wenye shaka na wanaotilia shaka imani ya wengine?

Katika mkutano na wajumbe wa wasomaji wa Qur’ani kutoka Haram Takatifu za Karbala mnamo Mei 5, 2026, Sayyid Ahmad al-Safi, Msimamizi wa Haram Takatifu ya Hazrat Abbas (AS), alisisitiza kuwa Msahafu wa Najaf ni jibu la kivitendo kwa baadhi ya shaka zilizozushwa dhidi ya wafuasi wa Ahl-ul-Bayt (AS) kuhusu Qur’ani Tukufu.

Alibainisha kuwa wazo la kuchapisha Msahafu wa Najaf lilianza mwaka 2009, na kazi hiyo imefanyika kwa miaka kadhaa iliyopita hadi kukamilika kwake katika mwezi mtukufu wa Ramadhan 1447 Hijiria, na kuzinduliwa katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam Ridha (AS) mwaka huu. Aliongeza kuwa Msahafu huu wa Kiiraqi, unaoubeba jina la Najaf al-Ashraf, ni muhimu kwa sababu unajibu baadhi ya shaka dhidi ya wapenzi wa Ahl-ul-Bayt (AS).

Qur’ani yenye utambulisho wa Kiiraqi

Msahafu wa Najaf umejitokeza kama Qur’ani ya kwanza yenye utambulisho kamili wa Kiiraqi kuanzia mwanzo hadi mwisho. Hii si nakala mpya tu; bali ni hati ya uhuru wa kisanaa. Imezalishwa kikamilifu na mikono na akili za Mashia wa Iraq, katika uandishi (khati), usanifu, na uchapishaji, ili kuthibitisha kwa ulimwengu kuwa Iraq, kama nchi ya elimu, ina uwezo wa kuzalisha Msahafu kwa kutumia khati asili ya Uthmani, inayotumiwa na Waislamu wote Mashariki na Magharibi kwa ajili ya ibada.

Uongozi wa Haram ya Hadhrat Abbas (AS) ulizingatia sana maelezo ya mradi huu mkuu, muhimu zaidi likiwa ni kumchagua mpiga-hati, Abdul Hussein al-Rikabi. Mpiga-hati huyu wa Kiiraqi ametajwa kama “mrithi wa wapiga-hati wakuu wa Baghdad”. Al-Rikabi aliandika herufi kwa ustadi uliounganisha wepesi wa kusomeka na uzuri wa kisanaa. Jitihada hii ya kisanaa ndiyo jibu fasaha zaidi kwa wale wanaodai kuwa Mashia wametengwa na huduma ya Qur’ani. Kila herufi katika Msahafu huu ni ushuhuda wa utiifu kwa aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Uhakiki makini na Baraka za Marjaa

Msahafu wa Najaf ulipitia mchakato mkali wa uhakiki wa kiufundi na kisayansi uliodumu kwa miaka mingi. Kamati za mahafidh na wasomaji wa Qur’ani na wanazuoni wa Hauza (Chuo cha Kidini) walipitia kila herufi na alama ili kuhakikisha inalingana kikamilifu na khati ya Uthmani.

Mchakato huu ulihitimishwa kwa baraka na kutambuliwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali al-Sistani, Marjaa au wanazuoni wa ngazi za juu wa Kishia nchini Iraq, ambaye aliutaja kuwa ni nakala yenye baraka, iliyohifadhiwa dhidi ya nyongeza au kasoro yoyote. Baraka hii haikuwa sifa tu; bali ilikuwa ni dhamana na hati ya kisheria inayokanusha uongo wote kuhusu kuwepo kwa “Qur’ani mbadala” na kusisitiza kuwa Msahafu wa Najaf ndiyo Qur’ani ile ile ya Muhammad (S.A.W) na Qur’ani ya Waislamu wote kutoka Mashariki hadi Magharibi na Kaskazini hadi Kusini mwa dunia.

Muunganiko wa Teknolojia na Utakatifu

Ili kukamilisha mradi huu, Uongozi haukujikita kwenye uzuri wa uandishi pekee, bali ulitumia teknolojia za kisasa zaidi katika kituo cha Dar al-Kafeel kwa ajili ya uchapishaji na usambazaji, ili kuzalisha Msahafu wenye sifa za kiulimwengu. Kutoka karatasi maalumu, wino rafiki wa mazingira, na mapambo ya kifahari, muunganiko huu wa teknolojia na utakatifu umefanya Qur’ani hii kuwa “alama ya karne”.

Ni zawadi kutoka Karbala na Najaf kwa ulimwengu wote, ikitangaza mwanzo wa zama mpya ambazo hakuna nafasi ya shaka kuhusu uaminifu wa wafuasi wa shule ya Ahl-ul-Bayt (AS) kwa Qur’ani Tukufu.

Msahafu wa Najaf ni Qur’ani ile ile Tukufu wanayosoma Waislamu wote, iliyoteremshwa kupitia Malaika mwaminifu Jibril (AS). Imeandikwa kwa mikono ya Wairaqi chini ya mwavuli wa Haram Takatifu ya Hazrat Abbas (AS), ili kuzifunga midomo ya wenye shaka na kuthibitisha kwa mafanikio haya kuwa Mashia, kama ndugu zao Waislamu duniani kote, ni walinzi na watumishi wa Qur’ani, na kwamba majaribio ya kuwatuhumu na kupotosha ukweli si chochote ila ni kama “mwangaza wa jangwani” unaodhaniwa kuwa maji, lakini unapofikiwa, unagundulika kuwa ni ukweli unaong’aa kama jua.

3497577

Habari zinazohusiana
captcha