Akihutubia kwenye Jukwaa la Mazungumzo la Tehran siku ya Jumapili mbele ya wageni kutoka mataifa na taasisi mbalimbali, Pezeshkian alieleza kuwa dunia ni kama nyumba ya pamoja kwa wanadamu wote.
“Dunia ni kama nyumba yetu sote, na kila mmoja ana haki ya kuishi ndani yake,” alisema. “Tukitambua kuwa dunia hii ni mali yetu sote, basi haki za kila mmoja zitaheshimiwa.”
Akinukuu aya ya Qur’ani Tukufu, “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.” (Surah Al-Hujurat, 49:13), Rais wa Iran amesisitiza umuhimu wa mshikamano unaovuka mipaka ya rangi, utaifa, au imani ya kimadhehebu.
Aidha, alikemea matumizi ya nguvu na dhulma katika mizozo ya kimataifa, akirejelea hasa vita vya Israel dhidi ya Gaza, ambapo watu zaidi ya 53,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto , wameuawa tangu Oktoba 2023.
“Kile ambacho Israel inafanya ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu. Utawala huu unawafukuza watu kwenye nyumba zao na kuendesha mauaji kila siku, halafu unazungumzia ubinadamu,” alisema Pezeshkian.
Kwingineko katika matamshi yake, Rais Pezeshkian amesema, Tehran kamwe haitaachana na mpango wake wa amani wa nyuklia. "Hatutaacha kamwe mpango wetu wa amani wa nyuklia, na hata wafanye nini, hatutakubali," amesema.
Rais Pezeshkian alikuwa akijibu matamshi ya hivi majuzi ya Trump kwamba, Marekani lazima ihakikishe Iran haipati silaha za nyuklia huku akitishia kuanzisha mashambulizi yanayolenga mpango wa nyuklia wa Iran.
"Kama binadamu, sitakubali kulazimishwa. Haijalishi wanatushinikiza kiasi gani, nakataa kutumiwa nguvu," rais wa Iran alisema.
Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo la Tehran unafanyika leo Jumapili na kesho Jumatatu, Mei 18 na 19, 2025 ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi. Wageni 200 kutoka nchi 53 duniani wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbalimbali pia wanashiriki katika mkutano huo.
Miongoni mwa washiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ni wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, jumbe kutoka nchi za Amerika ya Kaskazini, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Uturuki, Armenia, India, Japan, China, Russia, Saudi Arabia, Iraq na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, Mawaziri wa Mambo ya Nje, wawakilishi maalumu wa serikali.
3493137